Ads (728x90)

Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya mjini John Mwambigija akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Hotel ya Mbeya Peak leo asubuhi.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Esther Mpwiniza akifafanua jambo katika kikao na waandishi wa habari leo asubuhi


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mbeya mjini kimedai kuhujumiwa na chama kipya cha ACT kwa kutumia jina la chama hicho kujitangaza kwa wananchi na kupora wanachama wake.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa Habari jana katika Ukumbi wa Hotel ya Mbeya Peak Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya Mjini John Mwambigija alisema kuwa ACT kimekuwa kikifanya mikutano ya ndani huku kikijitambulisha kwa majina ya wajumbe wa Kitaifa wa chama hicho.
Alisema kuwa  hawazikubali mbinu zinazotumiwa na chama hicho na kuwa kitachukua hatua (hakuzitaja) iwapo kitaendelea kujitambulisha kwa wananchi kuwa wao ni sehemu ya CHADEMA.
‘’Wameitisha vikao Ukumbi wa Kiwira Motel, wamejitambulisha kuwa ni wajumbe wa Kitaifa kutoka CHADEMA, sisi hatuwatambui, lengo lao ni kutuvuruga, hatuwezi kukubali tutachukua hatua dhidi yao,’’alisema Mwambigija.
Aliffafanua kuwa taarifa zinazotolewa na viongozi wa chama hicho kuwa ndani ya CHADEMA kuna ufujaji wa fedha ni za uzushi na kuwa matumizi yote ya fedha za chama hicho yanaainishwa katika vikao vya utelekezaji kabla ya kupangiwa matumizi yake.
‘’Tuna vikao vya kupanga matumizi katika chaguzi mbalimbali,hata matumizi ya Helkopta tunapitisha kwenye vikao na tunakubaliana wajumbe wote wa mkutano, hao wanaohoji matumizi ya Chopa sisi hatuwatambui,’’alisema Mwambigija ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano mkuu wa Taifa wa chama hicho.
Katika hatua nyingine chama hicho kimesema kinajiandaa kwa uchaguzi mdogo wa kata ya Mwasanga Ntembela ambapo watamsimamisha mgombea atakayewakilisha vyama vitatu vinavyoungana katika Umoja ya Katiba ya Wananchi(UKAWA)
Akizungumzia uchaguzi huo Katibu Mwenezi wa chama hicho Mbeya mjini Baraka Mwakyabula alisema kuwa wamekubaliana kwa pamoja na vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF kuwa mgombea atakayesimama ataungwa mkono na vyama vyote.
Mkutano huo pia uliwahusisha viongozi wa chama hicho akiwemo Katibu wa Wilaya,Christopher Mwamsiku,Mwenyekiti wa BAWACHA Esther Mpwiniza,Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wilaya Saada Atiki, Kiongozi kamati ya ulinzi Jamal Juma na Mtunza hazina wa wilaya William Luvanda

Post a Comment