Ads (728x90)



Waziri wa Afya Dkt. Seif Rashid


Na Kibada Kibada, Katavi

Mkoa wa Katavi  kupitia sekta ya Afya  umewapatia watumishi   wa sekta hiyo wapatao 240  mafunzo  ya namna ya kutoa huduma ya Tiba  ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Katavi Dkt Yahaya Husein  ameeleza kuwa watumishi hao 240 waliopatiwa mafunzo ni sawa na asilimia 100 ya lengo lililowekwa  kuwapatia mafunzo ya huduma hiyo mkoani.
Akifafanua zaidi  Dkt. Husein amesema kuwa  hadi kufikia mwezi juni mwaka 2014 jumla ya vituo 61 sawa na asilimia miamoja na ishirini ya lengo  la vituo 51 vinatoa huduma hii katika Mkoa wa Katavi.
Amesema kuwa  ili kufanikisha adhima ya shirika la Afya Duniani la kuthibiti maambukizi toka kwa mama mwenye  VVU kwenda kwa Mtoto,Wizara ya Afya ikishirikiana na wadau wa Maendeleo imeanzisha huduma ya Tiba ya kuzuia  maambukizi toka kwa Mama mwenye VVU kwenda kwa Mtoto.
‘’Akina mama wajawazito wanaonyonyesha wakigundulika kuwa wana maabukizi ya UKIMWI wataanzishiwa tiba ya kudumu’’alisema.
Aidha kama Mkoa utahakikisha huduma hii inatolewa katika vituo vyote vinavyotoa huduma ya Afya ya Uzazi.
Kuhusu huduma   inayotolewa  amesema ni bora ,timu ya Afya Mkoa  na Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo katika sekta ya Afya Walter Reed zitaendelea kufanya ufuatiliaji na usimamizi elekezi kila mwezi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Programu ya Shirika la  Walter Reed Dkt Joseph Chintowa ameeleza kuwa Shirika lake kwa kushirikiana na  wadau wa wote wa Mkoa,Wilaya,Halmashauri na Mji wa Mpanda wanasaidia juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Dkt Chintowa ametoa wito kwa akina Baba kupima afya  pamoja na wake zao ili kujenga  familia zenye afya bora na ya uhakika,ambapo pia amewaasa wazazi kukumbuka dhamana waliyonayo juu ya kuwakinga watoto wao na maambukizi ya UKIMWI.

Post a Comment