Ads (728x90)

Utoaji huduma wa usafirishaji kwa magari binafsi umepewa ridhaa na vyombo vya dola baada mgomo wa daladala Jijini Mbeya hapa Askari Trafiki akiongoza magari yanayobeba abiria katika Stendi ya Daladala eneo la Kabwe


Bajaj zikichukua nafasi ya daladala zilizogoma katika utoaji wa huduma za usafirishaji Jijini Mbeya



Daladala pekee zinazoendelea kutoa huduma ni zile zinazoelekea Mwanjelwa, Mbalizi hadi TAZARA
Bajaj zikisubiri abiria baada ya daladala kugoma Jijini Mbeya
Magari aina ya Canter na Bajaj yameonekana yakitoa huduma za usafirishaji
Pilika pilika zikiendelea katika kituo cha Daladala cha Kabwe huku magari binafsi yakiendelea kutoa huduma kwa wananchi




SIKU tatu baada ya kuendelea kwa mgomo wa wasafirishaji wa abiria Daladala Jijini Mbeya, Sumatra kanda ya Mbeya imetoa onyo kwa wasafirishaji hao kwamba iwapo watandelea na mgomo wao zaidi ya siku ya kesho watafutiwa leseni zao.
Akizungumza kwa njia ya simu kutokea Jijini Dar es salaam, Meneja Sumatra kanda ya Mbeya Petro Chacha iwapo wasafirishaji hao wataendeleana mgomo wa kutoa huduma za usafirishaji katika Jiji la Mbeya hadi kesho, watalazimika kuwafutia leseni zao za usafirishaji wa abiria Jijini humo.
‘’Wameanza mgomo kwa madai ambayo si ya msingi, wao wanataka kuondolewa kwa route ya mzunguko kupitia Moon Dust na kutokea Soweto, kuingilia OilCom na kutokea Kabwe, hili limetusaidia kupunguza msongamano wa magari kati ya Mafiat hadi Soweto nyakati za jioni,’’alisema.
Alifafanua kuwa utaratibu huo ulipangwa baada ya vikao vya kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Mbeya baada ya kuona kuna kukwama kwa shughuli za kiuchumi katika Jiji la Mbeya kutokana na msongamano ambao umetokana na muingiliano wa magari yanayoenda safari ndefu na haya yanayosafiri ndani ya Jiji la Mbeya.
Chacha alisema kuwa kutokana na hali hiyo Sumatra iliweka utaratibu kuepusha msongamano na kuwa katika njia ambazo daladala zimekuwa zikipita kumekuwa na ongezeko la abiria ambao wanashuka na kupanda bila bugudha na hivyo kuongeza kipato kwa wasafirishaji hao na kuwa mgomo wao hauna sababu za msingi.
‘’Tumefanya utafiti wa kina tumebaini njia tulizoziongeza zimekuwa karibu na wananchi na Machinga, ambao awali walikuwa wakiweka bidhaa zao barabarani, kupeleka daladala upande huo tumewasaidia kuwafikia abiria wengi wanaofuata bidhaa kwa machinga waliohamishiwa upande huo,’’alisema Chacha.
Alibainisha kuwa baada ya kuibuka kwa mgomo huo baadhi ya magari binafsi na Bajaj zimeruhusiwa kubeba abiria ili kupunguza kadhia ya wananchi kukosa huduma hizo kwa kipindi ambacho Daladala zimeamua kugoma kusafirisha abiria.
‘’Tutatoa siku moja tu ya kesho kutwa iwapo wasafirishaji hao wataendeleza mgomo, tunawafutia leseni zao za usafirishaji wa abiria Jijini Mbeya,’’alisisitiza.
Mgomo huo wa Daladala umedaiwa kuitishwa na baadhi ya daladala zinazofanya shughuli zake kupitia njia za  Stendi Kuu na Uyole, Isyesye na Ituha hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa msongamano wa abiria wanaohitaji kuwahi shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo kuibuka kwa wasafirishaji mbadala wa Bajaj na magari binafsi ambayo ndiyo yanayotoa huduma za usafirishaji hadi sasa kumeondoa adha hiyo na kurejesha hali ya shughuli za wananchi kama kawaida.
Inaelezwa kuwa wasafirishaji waliogoma walihitaji kuongeza nauli kutoka Sh.400 ya kawaida hadi sh.500 kwa madai ya kufidia mzunguko ulioongezwa na Sumatra, na kwamba madai hayo ya ongezeko la nauli yanaweza kufidia gharama.
Aidha wakati magari yanayosafirisha abiria kwa njia za Uyole. Sokomatola na Stendni Kuu yameingia katika mgomo, yale yanayofanya safari kati ya Mbalizi, Sokomatola, Stendi Kuu na Mwanjelwa yanaendelea na utoaji wa huduma za usafirishaji kama kawaida.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mtandao huu wamedai kuwa ni vyema uamuzi mgumu ukachukuliwa dhidi ya watoaji huduma hao waliogoma ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao za usafirishaji na kwamba  Jiji la Mbeya linazidi kupanuka hivyo huduma zinahitajika katika maeneo ya pembeni badala ya kuendelea kung’ang’ania njia walizozoea awali.
Naye Mkazi wa Kabwe Jijini Mbeya alisema kuwa ni vyema wasafirishaji wakawa waelewa kwa kuwa Halmashauri ya Jiji inaendelea kupanuka hivyo ni muhimu wakajua kuwa kitendo hicho cha kuongeza safari za daladala ni kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Huduma za usafirishaji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya zinaendelea huku Bajaj, magari aina ya Noah, Canter, Landcruiser na Teksi zimekuwa ziwahudumia wananchi kwa nauli ya Sh. 500 kwa kila mtu kati ya Stendi kuu na Sae huku yale yanayoelekea Uyole yakitoza nauli ya Sh.600.

Post a Comment