Ads (728x90)Marehemu Adam Msyaliha aliyekuwa Mwenyekiti wa Programu ya Chadema Ni Msingi Mbeya mjini

Marehemu Adam Msyaliha enzi za uhai wake
 MWENEYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Programu ya ‘Chadema Ni Msingi’ Mbeya mjini Adam Msyalika(26) amefariki ghafla baada ya kuanguka bafuni nyumbani kwa baba yake mzazi Mzee Msalika eneo la Mabatini Jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa za Mwenyekiti wa Chadema Mbeya mjini John Mwambigija alisema kuwa marehemu ambaye pia alikuwa Katibu wa vijana wa jimbo la Mbeya mjini alianguka bafuni nyumbani kwa baba yake majira ya saa 5:00 asubuhi na baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Alisema kuwa alipofikishwa katika hospitali hiyo alilazwa katika wodi namba 11 ambako alipatiwa matibabu lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi kifo chake majira ya saa 5:20 siku iliyofuata.
Mwambigija alisema kuwa marehemu ambaye alikuwa ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere Jijini Dar es salaam ambako alipata Diploma ya Ofisa Uhusiano aliingia katika harakati za CHADEMA akiwa shule ya sekondari mwaka 2006 na kushika nyadhifa mbalimbali kwa ngazi ya Kata hadi mkoa.
Alisema ndani ya chama alikuwa ni kijana mchapakazi aliyeamini katika msimamo wake bila kuyumbishwa ikiwa ni pamoja na kuchangia mawazo yenye kukijenga chama hicho katika harakati mbalimbali za uongozi na chaguzi  mbalimbali za ndani na nje ya mkoa.
Naye Mwenyekiti wa Rasilimali na Fedha wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa chama hicho Lazaro Ngonyani alisema kuwa Marehemu ambaye alimaliza kidato cha sita katika sekondari ya Mlima Mbeya alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa chama hicho kuanzia mwaka 2006.
Ngonyani alisema kuwa marehemu kabla ya kuanguka alipata mshituko na kuanguka kisha akakimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya ambako ghafla alipooza upande wa kushoto na baadaye kufariki dunia akiwa katika harakati za matibabu.
Alisema marehemu anatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Kijijini kwao Iyula huko wilaya Mbozi mkoa wa Mbeya.

Post a Comment