Ads (728x90)


 Wadau wa Mfuko wa Bima ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya mkoani Katavi.

Na Kibada Kibada –Katavi.
ASILIMIA 78 ya wakazi wa mkoa mpya wa Katavi hawana Bima ya Afya kutokana na kile kilichodaiwa kuwa kuna ukiritimba wa utoaji huduma hiyo katika Hospitali na Zahanati mkoani humo.
Idadi hiyo imetokana na asilimia 12 pekee ya wakazi zaidi ya 500,00 wa mkoa huo ndio wanaopatiwa  huduma za mfuko wa Bima ya Afya ambao ni sawa na wakazi 66,000 waliojiunga na kutibiwa na mfuko huo.
Hayo yamebainika katika kikao cha Wadau wa mfuko wa Afya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wadau wa Mfuko wa Bima ya Afya na mfuko wa Hifadhi ya Jamii mkoani humo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Rajabu Rutengwe aliwaonya watoa huduma ya tiba kupitia mfuko huo kuacha ukiritimba na kuwabagua wagonjwa wenye vitambulisho vya Mfuko wa Bima ya Afya na kuwapa huduma wale wanaokuja na fedha taslimu.
Dkt. Rutengwe ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Mhandisi Emanuelo Kalobelo katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa mfuko wa Bima ya Afya kwenye ukumbi wa mikutano wa Katavi Resort alisema tatizo hilo ndilo linalosababishwa wananchi wengi kutojiunga na mfuko wa Bima ya Afya.
Alisema watoa huduma wa mfuko wa Bima ya Afya wamekuwa ni  kikwazo kinachowakatisha tamaa wananchi na kwamba mfuko wa bima afya upo kwa ajili ya kusaidia wananchi pale wanapokuwa wamejiunga katika mfuko wa hifadhi ya jamii na mfuko wa Bima ya Afya hasa kwa wale wananchi wasiokuwa na uwezo kuwa na fedha wakati wote.
Aliwataka  viongozi na wadau wa ngazi zote  kwa nafasi zao kuwahamasisha wananchi kujiunga katika mifuko ya bima ya Afya na Hifadhi ya jamii ili waweze kupatiwa matibabu bila matatizo.
Awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bima ya Afya Taifa Hamis Mdee alisema kuwa lengo  la taifa ni wananchi kujiunga na mifuko hiyo ilikuwa ifikapo mwaka 2015 waweze kufikia  asilimia 30 na kamba hadi kufikia machi 2014 wananchi waliojiunga na mfuko huo wapo asilimia 15  hivyo bado kuna changamoto na hamasa inayohitajika zaidi kwa wananchi kujiunga na mifuko hiyo.
Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho  walieleza kuwa uhaba wa dawa katika zahanati,vituo vya Afya na kwenye Hospitali ni tatizo linayowakatisha tamaa wananchi wanapoenda kutibiwa kwenye hospitali hizo.
Naye  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlele ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kibaoni Wilbroad Mayala aliomba utafutwe utaratibu utakaosaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa dawa ili kurejesha imani kwa wananchi iliyopotea katika mfuko huo wa bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii.

Post a Comment