Ads (728x90)Timu ya Green City ya Jijini Mbeya imefanikiwa kutwaa kombe la ‘kinywaji kinachotokana na kampuni ya TBL kinachodhamini mashindano ya timu yenye wachezaji 6 ya safari ya kuelekea Hispania baada ya kuichabanga Timu ya Savannah kutoka Mkoani Iringa kwa mabao 8-3.
Michuano hiyo ambayo ilichezwa katika Viwanja vya City Pub ulikuwa ni wa vuta nikuvute huku kila upande ukitaka kuchukua ubingwa wa kombe hilo kuungana na timu zingine nane Jijini Dar es salaam.
Timu itakayoshinda katika timu nane zitakazoshiriki mchuano huyo Leaders Club Jijini Dar es salaam itapata fursa ya kuelekea nchini Hispania kushuhudia ligi ya nchi hiyo.
Mchezo huo ambao huchezwa kwa dakika 20 na jumla ya wachezaji 6 ulihusisha timu nne kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Timu zilizoshiriki katika mchuano huo ni Green City na White Stars kutoka Jijini Mbeya,Savannah na Gaddafi kutoka Manispaa ya Iringa.
Green City ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo baada ya kuifunga timu ya Gaddafi mabao 9-0 wakati washindi wa pili Savannah ilifanikiwa kuingia fainali kwa kuifunga timu ya White Star ya Mbeya mabao 5-3.
Katika mchezo huo wa fainali magoli ya Green City yalifungwa na Issa Nelson aliyefunga magoli 3 Castro Litongwale aliyefunga magoli 3 na Lambert Lameck aliyefunga magoli 2.
Magoli ya Savannah yalifungwa na Enhard Mgeni magoli 2 na Johnson Ngogo Aliyefunga bao 1.
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa mshindi Meneja mauzo wa Kinywaji hicho Nyanda za Juu Kusini Vivianus Rwezaura alisema kuwa atatoa ushirikiano wa hali na mali kwa washindi ili wafanikiwe kuwa mabingwa wa Castle Lager Perfect 6.
Naye Meneja wa Kinywaji hicho Kabula Nshimo alisema kuwa mashindano hayo yameleta changamoto kwa washiriki na kwamba ana imani ushiriki wa timu hizo umeongeza ari kwa vijana kupenda soka.

Post a Comment